SCIENTIFIC AND ISLAMIC RESEARCHES

Fiqh/Sala

UTAFITI MBALIMBALI  KATIKA DINI NA SAYANSI

IMEANDALIWA NA  AL-AMIN ALI HAMAD

Mwenyeezi Mungu akipenda Mlango huu wa FIQH/TOHARA utakusanya Mafundisho ya Sala  ya Imamu Shafii. Tafsiri Ya Kitabu Cha Abi Shujaa.  Huu Ni mlango wa Pili. Mlango wa kwanza FIQH/TOHARA Ulimalizika na Ulikusanya Mafundisho ya Tohara.   Nia yangu ni kufanya kazi hii kila siku kidogo kidogo. Na nitaweka Tarehe katika kila Darasa kama nilivyofanya leo tarehe 28/06/2022.

27/06/2022

Alhamdulilah Leo  tutaanza safari yetu ya Kusoma mafundisho Ya  Abi Shujaa ambaye nilimwelezea kwa kifupi katika mlango wa FIQH/TOHARA. Marehemu Abi Shujaa (Baraka za Mwenyeezi Mungu Mtukufu Zimfikie) alifanya kazi kubwa ya Kuandika Sheria za Elimu ya FIQH kwa njia ya  kugawanya katika Mafungu na Milango mbalimbali baada ya kuitikia Mwito wa wanafunzi wake walipomuomba aiandike Elimu hii ya Imamu Shafii kwa njia iliyo Rahisi na Ya kueleweka.

Sheikh Abi Shujaa  ameanza kuuelezea mlango huu kwa Kusherehesha “Nyakati Za Swala” kwa kusema 

“Swala Tano Na Nyakati Zake”  

Swala Ya Adhuhuri

Akaanza na Swala ya Adhuhuri kwa kusema  “Swala ya Adhuhuri Ina Rakaa Nne. Na wakati wake wa kwanza ni Wakati  Jua linapokuwa katikati wakati wa mchana na kisha likianza kutua. Yaani Jua linapokuwa katikati kisha pale likianza kuzama upande wa pili au kwa lugha nzuri pale linapoanza kusogea upande wa pili. kwa kiingereza Tutatumia Neno  “Decline” Kwa kawaida  wakati Jua likianza kusogea mbele hapo litasababisha  Kivuli. Kwa hiyo kipindi hicho ndicho kinaitwa  DHUHURI  na mwisho wa kipindi hicho ni pale Kivuli cha kila kitu kifikie urefu sawa na Kitu hicho. Nadhani  imeeleweka. Yaani kipimo cha Kivuli ya kila kitu kikiwa sawa na Urefu wa kitu hicho basi ujue Swala yeyote baada ya hapo itakuwa nje ya nyakati za Dhuhuri. Hiki ni kipimo  kilichotumika hapo zamani enzi hizo wakati kulikuwa hakuna Saa na  pia hata leo unapokua mbali na misikiti na pia ukiwa huna Saa basi tumia Jua kama tulivyosoma mafundisho ya Shafii yanayotokana na Hadithi za Mtume ﷺ Utaangalia Jua na Kipimo cha Kivuli. Kwa lugha Rahisi  angalia Kivuli cha wakati wa Mchana. Urefu wa kivuli unapokuwa chini ya urefu wa kila kitu na hata kivuli chako mwenyewe basi huo ndiyo wakati wa Dhuhuri lakini unapozidi urefu wa chochote au hata kuvuli chako mwenyewe basi ujue Wakati wa Dhuhuri umepita.

Swala Ya Alasiri

Kwa hiyo Sheikh  wetu anaendelea kuelezea Swala Ya AL-ASR kwa kusema “Swala ya Al-Asr ni Rakaa Nne” Na wakati wake ni pale Kivuli  kinapozidi urefu wa kila kitu na hata kivuli chako mwenyewe. Ukisimama Nje katika jua angalia Kivuli chako mwenyewe ukiona urefu wa Kivuli umekupita basi ujue huo ndio mwanzo wa wakati wa Al-Asr.  Na  Sheikh Abu Shujaa anaendelea kusema kwamba Wakati unaopendeza kuswali  Swala ya  Al-Asr  ni  baada ya Kivuli cha urefu wa kila kitu kukizidi mpaka  kufikia urefu mara mbili yake.  Kwa mfano ukipima kivuli chako na ukiona urefu wa kivuli hicho kimefikia mara mbili ya urefu wako basi ujue wakati huo ndio karibu na mwisho wa Swala ya Al-Asr na baada ya urefu huo (wa Vivuli) inajuzu au inakubalika kuendelea kuswali Swala ya Al-Asr mpaka Jua litakapotua ijapokuwa siyo wakati Mzuri sana kama pale mwanzoni. Kwa hiyo Wakati wa Swala ya Al-Asr unaanza pale kivuli cha urefu wa jua kinapozidi urefu wako na wakati huo mzuri unaendelea  kiasi cha kivuli kukifikia urefu wako au chochote kile mara mbili. Baada ya hapo (Urefu wa Vivuli mara mbili) inajuzu (inakubalika) kuswali Swala ya Al-Asr kabla ya Kuzama Jua. Ninapozungumzia Vipimo vya Vivuli ni kivuli cha kila kitu siyo kivuli chako tu. Kwa mfano kivuli cha nyumba,  mawe, wanyama, na kila kitu. Nadhani imeeleweka.

Kwa Leo ninaishia hapa. Darasa lifuatalo litakuwa Swala Ya Maghrib, Ishaa na Asubuhi  Mwenyeezi Mungu akipenda. Kesho Darasa Litaendelea Mungu akipenda….

28/06/2022

Swala Ya Maghrib

Swala Ya Maghrib Ni Rakaa Tatu na Wakati wake ni Wakati Jua Limetua au Kuzama. Baada ya Hapo katika Muda wa Nusu Saa ambao unatosha kwa Kufanya Adhana, Kufanya Udhu, KuKimisha Swala na Kuswali. Na kipindi hicho ni Mpaka Kabla Ya Adhana Ya Swala Ya Ishaa.  

Swala Ya Ishaa 

Swala Ya Ishaa  Ni Rakaa Nne Na wakati wake wa mwanzo Mwanga wa Jua Mwekundu unapozama au kutoweka. Na Wakati wake unaendelea mpaka Theluthi Ya Usiku. Yaani  Ugawe Usiku katika Mafungu Matatu kisha Fungu la kwanza. Kwa mfano Ukiwa Usiku ni Masaa  Kumi Na Mbili basi Theluthi Ya Kwanza Ni Saa  Nne Usiku. Na Pia Inajuzu kuswali Swala Hiyo wakati wowote baada ya wakati huo mpaka kabla Ya Alfajiri. 

Swala Ya Asubuhi

Swala ya Asubuhi Ni wakati wa Alfajiri. Wakati wa Kiza na Mwanga. Yaani Katikati baina ya Kiza na Mwanga. Wakati huo unaendelea mpaka Mwanga unapolipunguza Kiza hilo. Yaani Mwanga unapoanza kuwa Mwingi kuliko Kiza. Na inajuzu (Inakubalika) baada ya Wakati huo kuswali katika  Wakati kabla ya Kutoka Jua. 

Kwa Leo ninaishia hapa. Darasa lifuatalo litahusu Masharti ya Kuwajibika kwa Swala na Swala Za Sunna. Mwenyeezi Mungu akipenda.

Darasa Litaendelea Mungu akipenda….

SHURUTI ZINAZOWAJIBIKA KATIKA SWALA

SWALA ZA SUNNA