SCIENTIFIC AND ISLAMIC RESEARCHES

Mazungumzo/Profesa-2

UTAFITI MBALIMBALI  KATIKA DINI NA SAYANSI

IMEANDALIWA NA  AL-AMIN ALI HAMAD

NAKUKARIBISHENI KATIKA SAFARI MBALIMBALI

MAZUNGUMZO BAINA YANGU NA PROFESA WA PHYSICS KATIKA CHUO KIKUU PARIS (FRANCE)

Alhamdulilah leo  Tarehe  17/09/2022  Wakati wa Jioni. Kuna utulivu na ni wakati mzuri sana  kuendelea  na kuandika  Mazungumzo yangu na Professor wa Physics ambaye asili yake ni kutoka Algeria. Kwa sasa Amestahafu na Nilifurahi sana kwamba alikubali makaribisho katika nyumba yangu. Mazungumzo  yetu yalikuwa kwa Lugha ya Kifaransa. Kama unavyoelewa Algeria ilitawaliwa na Wafaransa. Asili yake ni Mwarabu kutoka Algeria lakini anazungumza Kiarabu cha Lahaja ya Algeria na Pia Lugha yao Nyingineyo ambayo inaitwa Berber. Pia aliweza Kuzungumza Lugha ya Kiarabu Fasihi. Niliweza kuzungumza naye kwa Kiarabu cha Fasihi lakini amezoea sana Kifaransa na kila ninapoanza kuzungumza Kiarabu basi ananijibu Kifaransa kwani ameishi miaka  Mingi huko Ufaransa. Sikupendelea kumpa Taabu na kwa hiyo niliwasiliana naye kwa kifaransa. Namshukuru Mungu ninaizungumza Lugha Ya Kifaransa vizuri bila Tatizo.

Nilisoma mambo mengi yanayohusu Dini ya Kiislamu na Sayansi. Nilifurahi sana kukutana na  Mtaalamu kama huyu ambaye alikuwa Mwalimu  katika University ya Ufaransa inayojulikana kama Sorbourne mjini Paris kwa muda karibu Miaka zaidi ya 50.

Bwana huyu ana Experience ya Ualimu wa Sayansi  kwa muda mrefu na Somo alilokuwa akifundisha ni Physics.

Hapa chini  nimefasiri Mazungumzo  yangu na Profesa huyu kwa lugha ya Kiswahili. Kuna Ziyada na Pia Upungufu lakini Muhimu ni  Madhumuni. Nimenukulu  kila kitu ili utamu wa Mazungumzo usipotee.

Ijapokuwa Siku ya Leo kuna Utulivu  lakini kuna Watoto wa Majirani  ambao wanasukuma vile Vibaskeli  vidogo vidogo vya Gurudumu Moja na kwa hiyo kuna  Sauti hizo ambazo nimezizoea kwa sasa. Sehemu ambayo  Wanacheza ni Mbele ya Nyumba yangu. Sipendelei kuwakemea kwani watoto  wote wanafanya haya na mimi pia nilipokuwa mtoto  nilikuwa mtundu zaidi yao.

Nilipokuwa umri wao nilikuwa nikisukuma Matairi ya Baskeli ya Chuma Barabarani na Pia Matairi hayo yalikuwa na Ukelele  kuliko Matairi ya watoto hawa ambayo ni ya Mpira. 

Nilikuwa nikitengeneza Vigari vidogo  vidogo vya Miti na kutumia Gundi ya asili  kutoka katika Shina la Miti ya Gundi. Magari haya tulikuwa tukiyaburuza Barabarani kwa hatari kubwa kwani Magari pia yalikuwa yakitupitia. Tulifanya Utundu wa kila aina. Nakumbuka Tulipokuwa tukitembelea Mto  uliokuwa katika Kijiji changu. Mto huo una mchanga Mweupe kama ule wa Baharini na Hapo tulikuwa tukicheza Mipira. Na wakati mwingine tulikuwa tukicheza katika Mawe makubwa ya asili ambayo yalikuwa katikati ya mto kwa kutereza kuanzia juu mpaka chini. Wazazi na wazee wa Mji walitukataza tusiende katika Mto huo kwani wakati mwingine kuna Maji yanayoweza kuja kwa nguvu na maji haya yana nguvu sana. Yanapokuja huwa yamebeba mapande makubwa ya mawe na hata kuchukua Magari na Matrekta ambayo  yalijaribu kupita katika Mto huo.

Nakumbuka niliona kwa macho yangu  BASI lilokwama wakati maji yamejaa na watu  wanatoka madirishani kwa njia ya kamba. Nakumbuka pia kwamba Basi hilo lilizikwa na Maji chini ya Sakafu ya mto mpaka likapotea kabisa lakini watu wote waliokolewa kabla ya Basi hilo kupotea.. Siku moja niliona hapo karibu na mto Chui aliyekufa lakini Ngozi imeshachunwa na huyu aliuawa na watu kwa ajili ya ngozi.

Nakumbuka Sauti za Fisi  Usiku. Na pia Sauti ya Mto  unapojaa na kunguruma. Kwa kweli inatisha. Katika Kiji hicho kuna Mlima ambao  Wataalamu wanasema kuna Volcano na kwa hiyo huenda siku moja utapasuka na kwa hiyo watu wengi wanapotaka kujenga nyumba wanakwenda upande wa pili wa Kijiji kwani waliogopea ule Mlima utakapopasuka basi huenda ukamiminisha Lava ya moto katika Nyumba zao.

Kijiji Kidogo lakini Mengi ya Kuzumgumza. Nakumbuka kuna Daraja lililojengwa na Mjerumani alipokuwa Akitawala. Daraja hili halitumiki tena kwani  Limeharibika lakini limebaki hapo hapo na hakuna anayelitumia kwani ni hatari sana.

Kuna Kisima kinachobubujika Maji. Hapo zamani kisima hicho kilikuwa kidogo sana lakini miaka mingi imepita na sasa kimepanuka. Inasemekana kwamba tembo au ngombe aliwahi kuzama katika kisima hicho sijui kama habari hizi ni za kweli.

Tulikuwa tukipita karibu na kisima hicho wakati wa kwenda shule ya msingi kila siku  Asubuhi na Pia Tunaporudi Shule. Nakumbuka siku moja tuliona Nyoka Mkubwa Juu ya Mti karibu na Njia ya Kwenda Shule na Tukakimbia na kumjuulisha Mjomba wangu ambaye alikuwa na Bunduki zaidi ya moja Nyumbani kwake. Mjoma alikuwa anapenda kukusanya Bunduki na Kuzitundika Ukutani. Na siku hiyo alichukua Bunduki ya Bomba Mbili na kuja Kumuua Nyoka Yule. Alipiga Risasi Mbili na Mara Lile Joka likaanza Kujiachia Juu ya Mti na Mara Likaanguka Chini. Hakuna Aliyekwenda kuchunguza alipoangukia lakini nina hakika Risasi mbili zilimmaliza.

Kwa kweli  Maisha Ya utoto  yana Raha zake. Tulikuwa tukicheza  Kujificha na Kutafutana na katika Mchezo huo kuna wakati tulijificha Juu ya Miti. Tulikuwa Tukiitana.  “NJOO”  “NJOO” atakayekumata naye ndiye atakayejificha na wengine watamtafuta na hivyo hivyo. Hatuwasikilizi wazee wetu kwani tulikuwa tukienda miguu mitupu katika pori ambalo lina Miba.

Msomaji Samahani  Fikra zangu zimekwenda mbali Katika Utoto na nimesahau kuzungumza ile ziyara ya Profesa. Kwa kweli kuna mengi ya kuelezea ya utoto.

Sasa  Wakati umefika wa Kuwaletea yale Mazungumzo.

Ilikuwa  Asubuhi saa Tano wakati nilisikia Mlango  unagongwa na nilipofungua mara nikamuona Mzee aliyekuwa na Upara uliong’aa sana kama kwamba ametia  Mafuta. Mzee huyu alivaa mewani za Duara  kama vile  Mewani Za  Ghandi. Alikuwa na Tabasamu la Kuonyesha Furaha. Kwa kukisia Nilimpa Umri wa Miaka  75  au 80. Huyu ndiye Profesa  Mahmood ambaye nilijuana naye katika Chuo Kikuu. Profesa wangu Bwana Phillipson alikuwa Rafiki Yake na Hivi ndivyo nilivyomjua Bwana Huyu.

PROFESA: Asalaam Alaykum Kijana Wangu  Al-Amin

AL-AMIN ALI HAMAD: Alaykum Salaam Profesa

PROFESA:Nilifuata ulivyonielekeza na Alhamdulilah  sikupata taabu kuja kwako

AL-AMIN ALI HAMAD:Alhamdulilah Nashukuru Mungu  umefika Salama bila Tatizo. Na nimefurahi sana kwa kuitikia Makaribisho na kuweza kuja kwangu.

PROFESA:Al-Hamdulilah  Namshukuru Mungu

AL-AMIN ALI HAMAD: Profesa kabla ya chochote ningependelea kukukaribisha  kinywaji na chakula.

PROFESA:Maji ya kunywa yanatosha Asante sana.

AL-AMIN ALI HAMAD:Profesa leo ni mara ya kwanza kunizuru haiwezekani uondoke  bila ya kula chochote. Katika Nchi  yangu unapozuru nyumba ya mtu basi huwezi kuondoka bila ya kula chochote kwani utapewa chochote angalau Kahawa.

PROFESA: Asante sana sina budi kwa hiyo nitakula chochote ulichonacho.

AL-AMIN ALI HAMAD: Nitakutengenezea Chakula Cha Kitamaduni. Yaani Chakula Kinachoitwa Ugali na Mchuzi wa Samaki wa Nazi.

PROFESA: Asante sana. Kwa kweli sijawahi  kula chakula chenye jina hilo. Je Ugali ni  kitu gani?

AL-AMIN ALI HAMAD: Ugali ni Unga ambao unachamganywa na Maji na kisha Unasongwa. Ni Chakula kizuri sana kwa Afya. Ni cha Asili. Ni Chakula Safi. Wenye kukila wanakuwa na nguvu. lakini uwe macho kwani utakapokuja katika Nchi Yangu na Kula Ugali basi  utasahau huko  Arabuni na Pia unaweza kumsahau Mkewe na kujikuta unaoa Kwetu. Yaani kama umeoa basi usije kwetu.

PROFESA: hahahahaha  Al-Amin wewe Matata Sana.

AL-AMIN ALI HAMAD: karibu Profesa Chakula Tayari.

PROFESA: Alhamdulilah  Ugali na Samaki Tamu sana. Usipojiangalia unaweza kujiuma Vidole.

AL-AMIN ALI HAMAD: Ungepata Mboga Ya Mchicha na Kirumbu  ungeimba Nyimbo za Kiarabu zote.

PROFESA: HAHAHAHAHAHAHAHAHA (Profesa Anacheka)

AL-AMIN ALI  HAMAD: Profesa sasa tunywe kahawa na Tende.

PROFESA: Asante sana Mwenyeezi Mungu akupe  kila la kheri kwa kunikaribisha.

AL-AMIN ALI HAMAD: Mwenyeezi Mungu Akubariki kwa Kuja Nyumbani kwangu.

PROFESA:Nia Yangu leo tuzungumze mambo  mbalimbali.

AL-AMIN ALI HAMAD: Amin

PROFESA: Nitakuelezea Jambo  la kushangaza katika Kuruani Tukufu ambalo bado ninalifanyia utafiti.

AL-AMIN ALI HAMAD:Ningependelea kukusikiliza na nina hamu sana ya kusoma mapya.

PROFESA:Hapo  zamani  Waarabu na Mataifa Mengineyo ya wakati huo yalikuwa yakitumia Herufi  kuwakilisha Namba kwa mfano  Herufi  Alif Iliwakilisha  Namba 1, Herufi Baa Iliwakilisha Namba 2  na hivyo hivyo namba  zote tunazozijua leo ziliwakilishwa na Herufi. Hizi zilijulikana kama Thamni Za Herufi za Abjad

AL-AMIN ALIHAMAD: Naam Profesa

PROFESA: Sasa  tuone  Maajabu yafuatayo:

Abjad Ya  Neno  SURA + 21=Abjad Ya Neno  AMBIYAA + 10 + 11 + 12 + 14 + 31 + 47 +71

AL-AMIN ALI HAMAD:Bado  Sijaelewa. kwa kweli utafikiri kichina kwani inababaisha sana.hebu fafanua Profesa.

PROFESA:Pole Pole nitakufahamisha.

Neno  سورة  lina herufi  4

ukiligeuza katika  Values au Thamani ya Namba za hapo zamani utapata kama ifuatavyo:

Herufi  SIN=60     Herufi  Waw= 6  Herufi  Ra=200  Herufi  Taa Marboutta = 5

Tukijumlisha tutapata= 60 + 6 + 200 + 5=271

Kwa hiyo  Neno   سورة Thamani yake ni  271

Na tukifanya hivyo Hivyo  neno  الانبياء  tutapata Jumla ya Herufi  zake ni   96

sasa  tuzijumlishe  ili tuone ya kushangaza

Abjad Ya Neno SURA=271 + 21=Abjad Ya Neno AMBIYAA=96 + 10 + 11 + 12 + 14 + 31 + 47 +71

yaani

271 + 21 (Hii 21 Ni Namba ya Sura Ya Manabii katika Kuruani yaani  AL_AMBIYAA  au الانبياء  

Ngojea Nirahisishe Zaidi  Tumesema

271 + 21= 96 +10 + 11 + 12 + 14 + 31 + 47 + 71

271  ni  Thamani ya neno   SURA سورة 

21 ni Namba ya  Sura Ya Al-Ambiya الانبياء 

96  ni Thamani Ya  Neno Al-Ambiya الانبياء 

10  Ni Sura Ya  Nabii  Yunus

11 Ni Sura Ya  Nabii  Hud

12 Ni  Sura Ya Nabii Yusuf

14 Ni Sura Ya Nabii Ibrahim

Sura Namba 31 Ni Sura Ya  Luqman  au  Nabii  Luqman (Wanavyuoni wamegawanyika. Wengi wanasema alikuwa siyo Nabii lakini  Mtu wa Busara)

47  Ni Sura Ya  Nabii na Mtume Mohamad

71 Ni Sura Ya Ni Sura Ya Nabii Nuhu

Hizi Ni Jumla Ya Sura 7  ambazo zimeitwa majina ya Manabii. Kuhusu  Luqman  kuna Mgawanyiko. Waliosema kwamba ni Nabii wanahesabu Sura 7  na wanaosema kwamba alikuwa Mtu mwenye Busara basi wanahesabu Sura kuwa 6

Hebu  tuzilete tena zile Namba na kisha tuzijumlishe:

271 + 21= 96 +10 + 11 + 12 + 14 + 31 + 47 + 71

271 + 21=292  na 96 +10 + 11 + 12 + 14 + 31 + 47 + 71=292

Unaona ya Kushangaza.

Tunapata Namba zinazowiana. au  Balanced Equations

Kila Upande  una  292.

Je unaona ya Kushangaza.

Ngojea nifafanue zaidi:

Abjad Ya Neno SURA + 21=Abjad Ya Neno AMBIYAA + 10 + 11 + 12 + 14 + 31 + 47 +71

Mstari huu hapa Juu  ni sawa na Mstari hapa chini

271 + 21= 96 +10 + 11 + 12 + 14 + 31 + 47 + 71

Ni kama kusema:

Thamani ya Neno  SURA Kujumlisha Namba Ya Sura Ya AL_AMBIYAA  ni sawa na  Thamani ya Neno  Al-Ambiyaa  Kujumlisha  Sura Zote ambazo  zimetiwa majina Ya Mabii katika Kuruani Tukufu.

AL-AMIN ALI HAMAD: Profesa Kwa kweli  inashangaza lakini  inababaisha. Kwa nini jawabu ni  192? kwa nini  Jawabu kila upande linalingana?  kuna siri gani hapa?

Kinachotatanisha zaidi ni  Kuihesabu Sura Ya Luqman katika Sura Ya Manabii. Kwani  Wengi wanasema kwamba Luqman alikuwa siyo  Nabii lakini ni Mtu wa Busara. Tumesoma kwamba Kuruani imetaja Manabii  25 tu  sasa tukimhesabu Luqman kuwa Nabii  basi inakuwa Jumla ya Manabii kutajika katika Kuruani  ni  26.  Angalia  Mtatanisho. Lakini Ushahidi wa Kihesabu tuliouona hapa Juu wa Namba kulingana  unaonyesha kwamba Luqman alikuwa Nabii. Mbona  Hesabu Zinababaisha.

PROFESA: Elimu zetu bado changa na Kwa uwezo wake Mwenyeezi Mungu huenda kuna siku tutajua zaidi na ikiwa sisi hatutajua basi vizazi vya baadaye vitagundua mapya. Kwa sasa tuendelee kufanya utafiti. Kwa Kweli hapa ndiyo mwisho  wa Elimu yangu. Sijui zaidi, Kwa kweli namba zinashangaza sana. Na kwa upande mwingine Namba hizi  zinathibitisha kwamba Luqman alikuwa Nabii lakini  sina Uhakika. Mwenyeezi Mungu anajua zaidi. Allahu Akbar.

AL-AMIN ALI HAMAD: Profesa Mwenyeezi Mungu akubariki kwa Utafiti huu wa kiajabu. Ni Utafiti mzuri sana na huenda tukagundua  mengi  hapo baadaye. Utafiti  wako umeweka msingi wa ugunduzi wa baadaye. Allahu Akbar.  Profesa Je ungependa  Kahawa Nyingine na Tende?

PROFESA: Asante sana. Niletee na Tafadhali punguza kahawa isiwe kali kwani itanizuia nisilale vizuri kwani sasa jioni imeingia. Kuna Mengi tutazungumza ikiwezekana.

AL-AMIN ALI HAMAD: Profesa Tafadhali ikiwezekana Ulale kwangu  leo hii tupate Kuzungumza zaidi na Ukipenda Kesho  Pia je unaonaje?

PROFESA:Asante sana. Naona ni fikira nzuri sana. Leo Nitalala kwako na Ikiwezekana Tutazungumza Mengi Kwa uwezo wake Mwenyeezi Mungu

AL-AMIN ALI HAMAD: Asante Sana. Mwenyeezi Mungu akubariki.

PROFESA: Amin.

MAZUNGUMZO YANAENDELEA…………………….