UTAFITI MBALIMBALI KATIKA DINI NA SAYANSI
IMEANDALIWA NA AL-AMIN ALI HAMAD
BAADHI YA KAULI ZA IMAMU SHAFI
Ni Nani Imamu Shafi’ ?
Sheikh Huyu Anajulikana kwa Jina la Shaykh Al-islām Ni Mmoja wa Imamu Wanne wa Madhehebu Ya Sunni, Alikuwa Mwanafunzi wa Imamu Malik Ibn Anas na Pia ndiye alieanzisha Shule ya Madhehebu ya Shafii. Jina lake kwa Kirefu ni Abū ʿAbdullāh Muhammad ibn Idrīs al-Shāfiʿī. Imam Shafi’ alikuwa Mwandishi, Mwanachuoni wa Dini ya Kiislamu, Alichangia katika Sheria Za Elimu ya Fiqh (Islamic Jusrisprudence) Alizaliwa mwaka 767 (Chritian Era) Huko Gaza na kufariki Tarehe 20 January Mwaka 820 (Christian Era) Huko Egypt katika Mji wa Fustat.
KAULI 1
شَكَوْتُ إلَى وَكِيعٍ سُوءَ حِفْظِي
فَأرْشَدَنِي إلَى تَرْكِ المعَاصي
وَأخْبَرَنِي بأَنَّ العِلْمَ نُورٌ
ونورُ الله لايؤتى لعاصي
TAFSIRI
1/Nilishtaki kwa Wakii Kuhusu Udhaifu wa Kuhifadhi(Elimu)
I complained to Waki’ about my poor memory:
2/”Acha Maasi” Huu ndio Usia Alionipa
“Give up your sins!” was his advice to me;
3/Akanijuulisha Kwamba “Elimu ni Mwanga Kutoka kwa Mwenyeezi Mungu”
“For knowledge does not guide the sinner
4/Na Nuru ya Mwenyeezi Mungu haimuongozi Mwenye Kufanya Maasi
And the Light of God is veiled by iniquity.”
Inasemekana Kwamba Imamu Shafii alijikuta anaangalia Jambo la Asi kwa ghafla bila kutaka au kupenda mwenyewe na Kwa vile Asi lile lilikuwa likishughulisha fikra zake kwa muda alijikuta anashindwa kukumbuka Masuala muhimu ya Kidini na kwa hiyo akaenda kutaka Msaada wa Nasiha Kwa Mwalimu wake aliyekuwa anaitwa kwa Jina Waki’ Ibn Jarrah ambalo Kaburi lake lipo Cairo (Egypt) karibu na Msikiti wa Imam Shafii. Mashairi Hapa Chini huenda ni Kweli yanatokana na Imam Shafii na pia huenda sio kweli. (Yaani Hakuna Uhakika Kama ni Yeye aliyeyasema. Kuna Ushahidi Mbali Mbali ambao unathibitisha kwamba Hii ni kauli Yake Shafi’ lakini sio Muhimu aliyeyasema, Lililo Muhimu Ni Maana Ya maneno Haya. Kwa Kweli ni Nasiha Nzuri sana. Tukifuata itatusaidia katika maisha yetu.
KAULI 2
Binaadamu Wote Wamekufa isipokuwa Wale Wenye Elimu. Na Wote wenye Elimu Wamelala Isipokuwa Wale wenye Kutenda Mambo Mazuri, Na Wale wenye Kufanya Mazuri wamedanganyika Isipokuwa wale Walio na Ukweli (Sincere) na Wale Wenye Ukweli kila mara wapo katika Hali ya Wasiwasi.
KAULI 3
Unasema Kwamba wewe ni Mwili Tu, Lakini ndani yako kuna Kitu kikubwa kuliko Ulimwengu”
KAULI 4
“Moyo wangu umetulia kwa kuelewa kwamba jambo lililokadiriwa kulipata nitalipata, na lile ambalo sitalipata hilo halikukadiriwa liwe langu” –
KAULI 5
“Ajabu kubwa! Unatafuta Uongofu, Lakini hufuati Njia yake, Kwa hakika Merikebu haitangi (haitembei) katika ardhi kavu”
KAULI 6
“Elimu siyo kinachohifadhiwa. Elimu ni ile ambayo inaleta faida”
BAADHI YA KAULI ZA IMAMU ABU HANIFA
Ni Nani Imamu Abu Hanifa?
Abū Ḥanīfa al-Nuʿmān ibn Thābit b. Zūṭā ibn Marzubān, Kwa Kifupi Alijukikana kwa jina Abu Hanifa. Na Katika Waislamu wa madhehebu ya Sunni alijulikana kwa jina la Imamu Abu Hanifa. Asili yake ni Persia, Na aliishi katika Karne ya 8. Alianzisha Shule ya Madhehebu ya Hanafi Ambayo ilihusika na Masuala ya Kiislamu ya Elimu ya FIQH (Islamic Sunni Jurisprudence) Alizaliwa Tarehe 5 September Mwaka 699 (Christian Era) Katika Mji wa Kufa huko Iraq na Akafariki Tarehe 14 June Mwaka 767 Katika Mji wa Bagdad Huko Iraq. Kaburi lake lipo katika Msikiti wa Abu Hanifa huko Baghdad, Iraq
KAULI 1
Ni Nani sisi ambao Tunatamani pepo. Itatosha Mwenyeezi Mungu atuepushie Ghadhabu zake.
(Kauli hii ina maana kwamba Tumezidi maasi mengi na kwa hiyo angalau Mwenyeezi Mungu atuepushie Ghadhabu Zake).
KAULI 2
Hadithi Inapokuwa Sahihi basi hiyo ndiyo Madhehebu Yangu.
KAULI 3
Ni Kinyume cha Sheria Kwa Mtu Yeyote kukubali Maoni yangu bila ya kujua Asili yake Tumeyapata wapi.
KAULI 4
Tenda unayosoma kwani Nadharia bila ya Kitendo ni kama Mwili usio na Roho
KAULI 5
Mtu anayetafuta Elimu ili aipate Dunia atajikuta Elimu hiyo haina nafasi katika moyo wake.
KAULI 6
Matatizo ni Ni Matokeo ya Madhambi na Mtu Mwenye Madhambi hana haki ya kulalamika anapopata Matatizo.
KAULI 7
Vitendo Vichache Vya Kiakili vina Faida zaidi kuliko Vitendo Vingi Vya Ujinga
KAULI 8
Ukisoma Elimu Ya Kidini kwa Ajili ya Dunia Basi Elimu hiyo haitakaa Moyoni
INAENDELEA MUNGU AKIPENDA SIKU ZIJAZO, IPO KATIKA MAANDALIZI
BAADHI YA KAULI ZA IMAMU Malik ibn Anas
Ni Nani Imamu Malik ibn Anas?
Jina lake ni Mālik bin Anas bin Mālik bin Abī ʿĀmir bin ʿAmr bin Al-Ḥārith bin Ghaymān bin Khuthayn bin ʿAmr bin Al-Ḥārith al-Aṣbaḥī al-Madanī na kwa kifupi anajulikana kama Malik ibn Anas. Alizaliwa Madina mwaka 711 (Christian Era) ambayo ni sawa na Mwaka wa Kiislamu wa 93 (After Hijrah). Alifariki Mwaka 795 (Christian Era) Sawa na Mwaka wa Kiislamu wa 179 (After Hijrah) Umri wake ulikuwa Miaka baina ya 83 na 84. Aliishi katika Kipindi cha Abbasid Caliphate.Ni Kipindi cha tatu Cha Uislamu ambacho kilijulikana kama “Kipindi cha Dhahabu”. Elimu Mbalimbali za Kisayansi zilisomwa, Kuandikwa na kufanyiwa Utafiti katika wakati huo. Vitabu Mbalimbali vilifasiriwa kutoka Katika Lugha za Kigeni na kuandikwa katika Lugha ya Kiarabu. Na pia Kutoka katika Lugha Ya Kiarabu kwenda katika Lugha Nyinginezo kama vile Kigiriki. Imau Maliki Alikuwa Mwanachuoni aliyekusanya Elimu ambazo zilimpa Utukufu kama Jurist (Hakimu), Theologian (Shekhe) Na Traditionist (Mkusanyaji Wa Hadithi za Mtume Mohamad ﷺ). Alizaliwa huko Madina (Saudi Arabia). Alijulikana kama Imamu wa Madina. Aliamini na Kufuata Njia ya Ijtihad katika Kutatua Masuala ya Kidini katika wakati huo. ijtihad ni kutumia Fikra. Kinyume na “Taqliyd” ambayo Inahusu Kukopi Majibu ya Masuala au Fatwa ya Kidini zilizopita ambazo zilitolewa na wanavyuoni waliotangulia na walioaminiwa. Interest yake kubwa ilikuwa Elimu ya FIQH (Jurisprudence) yaani Sheria za Dini katika Milango mbalimbali kama vile Sala, Saumu, Zakah, Hija, Ndoa na Mengi Mengineyo. Na Pia Elimu ya Hadithi. (Science ya Hadithi za Mtume ﷺ) alizokusanya katika Kitabu chake maarufu cha Al-Muwatta. Imamu Maliki alianzisha Madhehebu au Shule Ya Madhehebu ya Maliki (Jina la Madhehebu yanatokana na Jina Lake). Imamu Maliki alikuwa Sunni kama vile Imamu Shafii na wengineo. Madhehebu yake ni Miongoni mwa Madhehebu Manne Maarufu ya Sunni.
KAULI 1
Mimi ni Binaadamu na kuna wakati ambao katika kutoa Maoni Yangu ninafanya Makosa na wakati mwingine Sifanyi Makosa. Kwa hiyo Chunguzeni Maoni Yangu na Ukubali yanayokubaliana na Kuruani na Sunnah (Hadithi za Mtume) Na Uache chochote ambacho (Maoni Yangu kinakwenda kinyume na Sunnah (Hadithi za Mtume).
KAULI 2
Hakika Elimu hii ni Miili na Damu Zenu, Mtaulizwa juu yake Siku ya Kiyama. Basi angalieni (kuweni Macho) kwa nani mnaichukua.
KAULI 3
Hakika mtu anapoanza kujisifu, basi utukufu wake utamtoka.
KAULI 4
Ishara ya uovu wa mtu ni hitaji lake la kubishana kila wakati.
KAULI 5
Nimekutana na watu katika mji wangu ambao wanaonekana kuwa waadilifu zaidi lakini walitoka na kuanza kufichua makosa ya wenzao hivyo Mwenyezi Mungu akaweka wazi makosa yao. Najua Pia watu wengine ambao wana makosa lakini kwa sababu wao ni wakimya Mwenyezi Mungu huwafanya watu wasahau makosa yao.
KAULI 6
Ninapoulizwa Masuali (Fatwa) Ya Kidini basi ninakosa usingiziUsiku na Mchana (Siku zaidi ya Moja).
KAULI 7
Sikuanza kutoa Fatwa (Kujibu Masuala Makubwa ya Kidini) Mpaka Manavyuoni karibu Sabini waliposema kwamba Nitaweza Kujibu Masuala Hayo. (Yaani Walininasihi na Kuniruhusu)
KAULI 8
“Usiwape watu waliopotea (wajinga) kukaribia masikio yako . (Kwa Mazungumzo ya Upuzi) Hujui ni aina gani ya shida inayoweza kuleta ndani yako.”
KAULI 9
Ikiwa nina sababu 99 za kuamini kuwa mtu fulani ni kafiri na sababu moja tu ya kuamini kwamba mtu huyo siyo Kafiri, Ningependelea Imani au Fikira ya Pili.
(Kauli hii Ina maana kwamba Yaani Siyo vizuri kumpa sifa ya Ukafiri mtu bila kuwa na Uhakika wowote).
KAULI 10
Ibn Battaal amesema: ‘Imam Malik aliulizwa: Baba yangu ananiomba nifanye jambo fulani lakini mama yangu ananizuia. Imam Malik akajibu: “Mtii baba yako na usimwasi mama yako.
KAULI 11
Mama yangu alikuwa akinivisha nguo za wanachuoni nikiwa bado mvulana mdogo na alikuwa akiniambia ‘Nenda Msikitini utafute elimu kutoka kwa Imam Ar-Rabi’ah, usome adabu zake kabla ya kuchukua Elimu yake.
KAULI 12
Daima kuwa katika kundi linayokuhimiza kuelekea mwelekeo mzuri.
(Yaani jiepushe na Makundi yanayohimiza watu kuelekea mwelekeo mbaya.
KAULI 13
Tafuteni Elimu, Angalau Inayohusu kuvaa viatu kwa mujibu wa Sunnah”
(Yaani Tusidharau Elimu yoyote angalau ndogo kama vile kuvaa kiatu)
KAULI 14
Mwenye ujuzi asiache kutafuta maarifa.
(Yaani Elimu haina mwisho na kwa hiyo hata ukajiona una Elimu kubwa usiache kuendelea kutafuta Elimu)
KAULI 15
Unapofanya Upuuzi wowote na chochote duniani tahadhari sana usifanye Upuuzi na Dini.
KAULI 16
Sunnah ni kama jahazi la Nabii Nuhu. Atakayeingia ndani yake anapata wokovu, na anayekataa atazama.
KAULI 17
Sio Elimu ndiyo inapaswa kukujieni bali ni nyinyi ambao mnapaswa kuijia Elimu.
(Yaani Elimu itafutwe kwa juhudi na wala usisubiri ikufuate)
KAULI 18
Sio faida kwa mtu yeyote mwenye Elimu kuacha Kuendelea kujifunza
KAULI 19
Elimu Siyo kujua idadi kubwa ya maandishi na Kunukulu Masimulizi tu peke yake bali ni Nuru ambayo Mwenyezi Mungu huiweka moyoni
KAULI 20
Muumini ni kama lulu; popote alipo, uzuri wake (sifa zake) uko pamoja naye
BAADHI YA KAULI ZA IMAMU Aḥmad ibn Ḥanbal (أَحْمَد ابْن حَنۢبَل), au Ibn Ḥanbal
Ni Nani Imamu Aḥmad ibn Ḥanbal (أَحْمَد ابْن حَنۢبَل), au Ibn Ḥanbal ?
Imamu Ibn Hambal alizaliwa mwaka 780 Katika kipindi cha Christian Era, Tarehe ambayo inalingana na Tarehe ya kiislamu Mwezi wa Rabi-ul-Awwal Mwaka wa 164 Baada ya Hijra Katika mji wa Baghdad (Iraqi). Katika kipindi maarufu cha Elimu na Sayansi kinachokulikana kama Kipindi cha Dhahabu kutokana na Elimu Za Sayansi na Nyinginezo. Ni Enzi Ya Utawala wa Abbassid Chaliphate. Alikuwa Expert Katika Sheria Za FIQH (Muslim Jurist) Expert katika Elimu ya Dini(Theologian) Walii kwani aliitupa Dunia kwa ajili ya Dini(Ascetic), Alikuwa Expert katika Elimu za Sunna za Mtume. Mohamad ﷺ (Hadith Traditionist). Inasemekana kwamba katika Maisha Yake aliwahi kuwa Hakimu (Judge) Huko Isfahan (Iran).Na ndiye aliyeanzisha Shule au Madhehebu ya Sunni inayojulikana kwa Jina lake mwenyewe kama “Madhehebu Ya Hambali” (Ni Mojawapo Ya Madhehebu au Mashule Manne Ya Sunni katika Uislamu yaani Miongoni mwa Madhehebu ya Shafii, Maliki, na Hanafi). Kitabu chake alichokusanya Hadithi za Mtume Mohamad ﷺ ni Maarufu sana Duniani kinajulikana kwa Jina kama “Musnad” na pia aliandika vitabu vinginevyo kama vile Radd ʿala’l-Ḏj̲ahmiyya wa’l-Zanādiḳa
Alisoma Elimu za Sunna Za Mtume (Hadith) kutoka kwa Wanavyuoni Mbalimbali. Na Katika Kipindi chake alikataa kukubaliana na Imani za Madhehebu ya Muutazilites ambayo ilikuwa ni chombo cha Dini ambacho kiliwakilisha Utawala wa Khalifa (Amir) Maa’mun katika wakati huo. Madhehebu haya ya Muutazilites yaliamini kwamba Kuruani Imeumbwa na Mwenyeezi Mungu. Hambali hakukubali Imani hii na hakuogopa Utawala wa Amir Maamun. Kutokubali Imani hiyo ilisababisha kutiwa Jela. Kipindi cha A-Maamun kilipita na Imamu alikuwa bado Jela. Kipindi kilichofuata ni cha Al-Muttasim. Huyu Al-Muttasim alimtesa sana Imamu Hambal na Miongoni mwa Mateso ilikuwa kupigwa Viboko vikubwa mpaka ikafikia Wananchi Kupiga makelele. Baada ya Wananchi kufanya Ghasia hiyo ilibidi aachiwe Huru. Baada ya Kiongozi wa tatu aliyejulikana kwa jina kama Al-Wathiq kuchukua Madaraka ya Ukhalifa aliendelea na siasa yake ya Kufuata Imani za Muutazilites kama Makhalifa waliotangulia (Al-Maamun na Al-Muttasim). na Aliona lililo bora ni Kumfukuza Imam Hambali Hapo Baghdad. Utawala uliofuata ulikuwa wa Al-Muttawakil aliyekuwa Ndugu yake Al-Wathiq, Huyu alikuwa na Imani za kimaendeleo na za Sunni. (Traditional Sunni beliefs) Na Ibn Hambal Akakaribishwa arudi Baghdad.
Imani zake zimeathiri Wanavyuoni wengineo kama vile Ibn Taymiyyah na pia Vikundi vya kidini kama vIle Wahabbi na Salafism huko Saudi Arabia Ijapokuwa Kuna wengi amba hawakubaliani na Habari Hizi. Aliamini Kufutu Maswali Makubwa ya Kidini kwa Kutafuta na kutumia Juhudi (Ijtihad) na Alikataa Kunukulu Maswala Yaliyofutuliwa Katika Enzi zilizopita. (Taqliyd).
Alikuwa Mufti katika umri mdogo sana. Na leo tunakuta Madhehebu hii inafuatwa huko Saudi Arabia, Qatar na United Arab Emirates.
Ukilinganisha na Madhehebu Matatu kama vile Hanafi, Maliki na Shafi utakuta Hambali ni pekee katika kufuata Madhehebu za zamani kama vile “Athari” ambayo iliamini Yaliyo dhahiri tu (Literal Meaning) katika kuifasiri Kuruani na Kujiepusha na Ya Undani kwa kutumia Elimu za Balagha (Metaphorical Meanings) na hasa Sifa za Mwenyeezi Mungu. Kwani Kufanya hivyo hatutapata ukweli. Waliamini kwamba Kutumia Fikira (Rationalism) ni Hatari kubwa kwani Binaadamu hatuwezi kufikia kuelewa Undani wa Aya Za Kuruani kwa Kutumia Akili.
KAULI 1
Ikiwa nyinyi mnataka Mwenyezi Mungu aendelee kukupeni mambo mnayoyapenda, basi dumuni katika kufanya yale Anayoyapenda (Mwenyezi Mungu)
KAULI 2
Ikiwa nyinyi mnasema kuwa ni miongoni mwa wale wanaojikinga na Moto na wanataka Pepo, basi jitahidini kwa hayo mnayoyatafuta na wala msipotoshwe na matamanio yenu ya dunia.
KAULI 3
Kama majaaliwa yanawasilishwa (yanaonyeshwa) kwa mtu basi angechagua yule ambaye Mwenyezi Mungu amemchagulia.
KAULI 4
Misingi ya Sunnah kwetu sisi ni: Kushikamana na yale waliyokuwa wakifuata Maswahabah wa Allaah (Swalla Allaahu Alayhi wa Aalihi wa Sallam) na kuwachukulia kuwa ni mifano ya kuigwa, na kuacha uzushi, kwani uzushi wote ni upotofu.
KAULI 5
Iwapo mtu atakuletea Salaam kutoka kwa mtu, basi inapendekezwa kujibu: ‘Alayka wa ‘Alayhi salaam. (Yaani Kwako wewe na Yeye Salaam Pia)
KAULI 6
Mwenye kukataa HadithI ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu Alayhi wa Aalihi wa Sallam) basi yuko kwenye ukingo wa maangamizo.
KAULI 7
Muziki husababisha unafiki kuchipuka na kukua moyoni.
KAULI 8
Ibn Taymiyah Ananukuu: Imaam Ahmad bin Hanbal amesema: “Jihadharini na kuendekeza mtazamo wa kusema kwamba haujawahi kuusikia kutoka kwa mwanachuoni yeyote.
KAULI 9
Imam Abu Dâwûd Al-Sijistânî amesema: ”Imam Ahmad.ibn Hanbal hakuwahi kujihusisha na mambo ya dunia ambayo kwa kawaida watu wanajihusisha nayo; lakini inapotajwa elimu alikuwa katika mstari wa mbele kuzungumza.
KAULI 10
Al-Maymooni alisema: Ahmad bin Hanbal aliniambia: Ewe Abu’l-Hasan, ukiona mtu anamsema vibaya Sahaabah yoyote, basi uwe na shaka juu ya Uislamu wake.
KAULI 11
Wapendeni watu wa Sunnah kufuatana na Kiwango Chao Cha Sunnah.
KAULI 12
Niliacha kujaribu kuwafurahisha watu na kuanzia wakati huo nilipata nguvu niliyohitaji katika kusema ukweli.
KAULI 13
Msifuate maoni yangu; wala msifuate rai ya Maalik, wala Shaafi’iy, wala Awzaa’iy, wala Thawri, bali chukueni huko walikochukua hao na Nilikochukua mimi.
KAULI 14
Rai ya Awzaa’iy, Rai ya Maalik, Rai ya Abu Haniyfah: zote ni Rai, na zote ni sawa machoni pangu. Hata hivyo, dalili ni katika Riwaya (kutoka kwa Mtume Mohamad ﷺ na Maswahabah zake.
KAULI 15
Watu wanahitaji ujuzi zaidi kuliko kuhitaji chakula na vinywaji, kwa sababu wanahitaji chakula na vinywaji mara mbili au tatu kwa siku, lakini wanahitaji ujuzi wakati wote.
KAULI 16
Uzushi umeenea, na asiyekuwa na Sunnah au Riwaya, (Sunnah za Mtume ﷺ) basi ataingia kwenye uzushi.
KAULI 17
Nilimuabudu Mwenyezi Mungu miaka 50 na sikupata utamu wa kuabudu mpaka nilipoacha vitu 3
1.Niliacha kupendeza (Kuwasifu)watu na nikapata nguvu ya kuzungumza ukweli,
2.Niliacha kundi la watu waovu nikapata kundi la watu wema
3.Niliacha utamu wa Dunia nikapata utamu wa akhera.
KAULI 18
Tenda wema, kwani utakuwa katika hali nzuri siku zote maadamu unakusudia mema.
KAULI 19
Siku zangu bora zaidi ni wakati ninapoamka na kuliona kabati langu halina chochote. Kwani hiyo ndiyo siku imekamilika kwangu kumtegemea Mwenyezi Mungu.
(Yaani Kabati lisilo na chochote ina maana hakuna chakula na vinginevyo vya maisha. Imani ndiyo izidi kwa kumtegemea Mola, usibabaike na mitihani midogo au mikubwa kwani Mungu yupo na yupo katika kupima imani yako)
KAULI 20
Imam Ahmad bin Hanbal Rahimahullah aliulizwa; “Kwa nini hutumii kukaa wakati mwingi na watu?” Yeye Rahimahullah akajibu; “Kwa sababu sipendi kuaga.
KAULI 21
Sikuwahi kuandika hadith hata moja isipokuwa niliifanyia kazi hadi nikapata Riwaya kwamba Mtume ﷺ alitibiwa kwa njia ya Cupping (Cupping Therapy au Tiba Ya Vikombe) na akampa Abu Taybah aliyemtibu malipo ya dinari moja Kwa hivyo, na Mimi nikafanya Tiba Hiyo na kumpa Aliyenitibu Malipo ya dinari.
KAULI 22
Ni jambo la kustaajabisha sana kuwa katika kuendelea kughafilika, mkifuata matamanio yasiyo na faida mkipoteza muda wenu kwa kupuuza jambo hili muhimu zaidi (Yaani Dini).(Msisahau Kwamba) Mnasukumwa kwa mwendo mkali (kuelekea kifo) mchana na usiku, saa baada ya. saa, kama kupepesa kwa jicho.”
KAULI 23
Haiwezekani hata kidogo Mwenyeezi Mungu (Allah) Kufananishwa na chochote zaidi ya yale Aliyojipambanua kwayo Yaani Mwenye Enzi Na Mkubwa.
KAULI 24
Kwa kila jambo kuna baraka; baraka za nyoyo ni kuwa radhi kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu, Mwenye Utukufu.
KAULI 25.
Ikiwa nyinyi mnapenda Mwenyezi Mungu akuwekeni juu ya kile mnachokipenda, basi bakieni juu ya kile anachokipenda, na kheri ni kwa yule asiyeona kheri nafsini mwake.” (ili uendelee kufanya mazuri daima na usitosheke katika kujifikiri kwamba umejaa mazuri na hakuna haja ya kuendelea na juhudi hizo)
KAULI 26
Ahmad bin Hanbal Aliambiwa: “Hakika baadhi ya watu hukaa pamoja na watu wa Bida’a” Ahmad bin Hanbal akasema: “Muwashauri.”Yule mtu akajibu: “Lakini alikataa ushauri huo”.Ahmad akasema: “Wahesabuni miongoni mwao”
KAULI 27
Salih mtoto wa Imam Ahmed Ibn Hanbal alisema; “Wakati wowote mtu mwadilifu, mcha Mungu ambaye hakughururika na Marembo Ya Ulimwengu huu anapokuja kumtembelea baba yangu basi Baba Yangu aliniita ili nimuone kwani alipendelea niwe kama huyo.”
KAULI 28
Watu wanahitaji upole na wema. Ni bora kuamrisha mema bila ya ukali, isipokuwa mtu ambaye anafanya uovu waziwazi, ambaye lazima aambiwe na kusimamishwa (kwa ukali)”
KAULI 29
Msimulie Allaah kwa yale Aliyojipambanua nayo, na Usisimulie Yale ambayo Allah Amejikanushia Nayo.
KAULI 30
Jishughulishe na kila jambo jema na fanya hima kulitenda kabla halijakuzuia Jambo lingine kufanya hivyo.
KAULI 31
Misingi wa Misingi Ya Sunnah kwa mtazamo wetu ni: Kushikamana na njia ya Maswahabah wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kufuata mfano wao na kuacha bid’ah, kwani kila bid’ah ni upotevu (Bid’ah ni Jambo Jipya katika Dini aliyokuja nayo Mtume Mohamad ﷺ
KAULI 32
Watu wote wanapaswa kumtegemea Mwenyezi Mungu, lakini (Wafanye Kazi ili)wapate riziki zao pia. (Yaani Usimtegemee Mwenyeezi Mungu bila kufanya kazi yeyote)
KAULI 33
Elimu ni kama pesa, kadiri unavyomiliki zaidi ndivyo unavyopaswa kulipa Zakati zaidi. (Yaani mfano wa pesa na kulipa Zakah kufuatana na Kadiri ya mali unayomiliki basi kadiri unavyopata Elimu na ndiyo hivyo hivyo Unakuwa na Madaraka Zaidi)
KAULI 34
Kuhusu ugumu wa kuwakosoa wazushi, Ibn Taymiyyah (Rahimahullaah) alirejelea nukuu ifuatayo: “Baadhi ya watu walipomwambia Imaam Ahmad Ibn Hanbal (Rahimahullaah) kwamba wamekosa raha katika kuwakosoa watu, alijibu, ‘Ikiwa utanyamaza na mimi nikanyamaza, basi ni nani atakayemfahamisha mjahili Tofauti baina ya jambo lililo Sahihi na lile lenye dosari?
KAULI 35
Kwa hakika, Imaam Ahmad bin Hanbal alipoulizwa kuhusu mtu aliyefunga, akaswali na kujitenga msikitini kwa ajili ya ibada kama alikuwa kipenzi zaidi kwake kuliko mtu aliyewakemea Ahlul-bid’ah (wazushi), alijibu: “Anapofunga na kuswali na kujitenga, basi anafanya hivyo kwa manufaa ya nafsi yake. Lakini anapozungumza dhidi ya wazushi, anafanya hivyo kwa manufaa ya Waislamu kwa ujumla, na hili ni kheri zaidi.
INAENDELEA MUNGU AKIPENDA SIKU ZIJAZO, IPO KATIKA MAANDALIZI